facebook likes

Monday, September 23, 2013

Wanafunzi wa zamani saidieni shule zenu mlizosoma


Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akizungumza na waliokuwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Weruweru, iliyoko mkoani Kilimanjaro, wakati wa maadhimisho ya miaka 50 ya kuanzishwa kwa shule hiyo.
SOMA ZAIDI.....
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, amewataka Watanzania kuiga mfano wa Shule ya Sekondari Weruweru ambao wahitimu wake wa zamani (Alumnae), wameamua kuchangisha fedha na kukarabati shule yao ya zamani.

 Alitoa wito huo mwishoni mwa wiki wakati iliyopita akizungumza na mamia ya wanajumuiya waliohitimu katika shule hiyo (Alumnae), wanafunzi waliopo pamoja na wageni mbalimbali waliohudhuria sherehe za Jubilei ya miaka 50 ya Shule ya Sekondari ya Wasichana Weruweru.


Waziri Mkuu ambaye alikuwa mgeni rasmi katika sherehe hizo alisema: “Watanzania wengi tuna nafasi za kuchangia shule zilizotusomesha. Tuige mfano wa wenzetu wa Weruweru, tukutane na kusaidia shule tulizosoma."

Alisema yeye alisoma Shule ya Sekondari Pugu kati ya mwaka 1965 na 1967, lakini kumekuwa na juhudi mbalimbali za kuwakutanisha wahitimu wa shule hiyo ambazo hazijawahi kufanikiwa.

“Ninawataka mtembee kifua mbele kwa sababu shule yenu imezaa matunda mazuri sana,” alisema huku akiwasifia wana Weruweru waliohitimu zamani kwa kuamua kuja na wazo hilo jema la kukarabati shule yao ya zamani.

Mapema, akisoma taarifa ya shule hiyo, Mwalimu Mkuu wa Weruweru, Rosalia Frimini, alisema shule hiyo iliyoanzishwa Oktoba 22, 1963 hivi sasa ina wanafunzi 570 wa kidato cha tano na sita tu wanaosoma michepuo ya PCB, EGM,ECA, HGE, HGK na HKL.

Alisema shule hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo uchakavu wa maabara, madarasa, mabweni na mifumo ya umeme.

Alisema shule hiyo ina upungufu wa watumishi wakiwemo manesi, wapishi, mkutubi na walinzi.

“Shule pia inakabiliwa na tatizo la usafiri.  Landrover 110 iliyopo shuleni ni ya tangu miaka ya 80 na matengenezo yamekuwa makubwa, tunaomba utusaidie kutatua tatizo la usafiri... tunapata shida hasa ikitokea watoto wanaumwa na wanatakiwa kupelekwa hospitali ya mkoa,” alisema.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dk. Maria Kamm, ambaye aliongoza shule hiyo kwa miaka 22 kuanzia mwaka 1970 hadi 1992, aliiomba serikali irudishe mfumo wa kidato cha kwanza hadi cha nne kwa shule kongwe ambao ulifutwa na serikali.

Alisema katika kujenga maadili kwa watoto, inabidi waanze tangu wanapoingia sekondari.

Alisema Sera ya Taifa ya Elimu ya Kujitegemea ilikuwa ndiyo siri kubwa ya kuwaumba wasichana waliopitia shuleni hapo na kwamba ilileta usawa na kuondoa ubaguzi.

Naye Naibu Katibu Mkuu mstaafu wa Umoja wa Mataifa, Dk. Asha-Rose Migiro, ambaye ni mhitimu wa shule hiyo alisema Jubilei ya miaka 50 ya Weruweru ni sehemu ya kusherehekea ndoto iliyotimia na ndoto iliyokuwa kweli kwa wanafunzi wengi waliosoma kwenye shule hiyo.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

COMMENTS

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...