HUWEZI kutawala miili ya watu ukaacha mioyo yao. Ndiyo, mjumbe hauawi, ni kauli ya hekima ya tangu enzi za wahenga wetu.
Leo ni mwaka mmoja tangu mwandishi wa habari na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wandishi wa Habari mkoani Iringa,Daud Mwangosi kuawa.
Ilikuwa ni Jumapili ya Septemba 2, 2012. Hakika, siku ile itabaki katika kumbukumbu za Watanzania kwa mamilioni. Ni kwa kufikiwa na taarifa za kutisha za mauaji ya mwandishi wa habari. Haya yanaingia katika historia kuwa ni mauaji ya kwanza kwa mwandishi wa habari kufanyika hadharani tangu nchi hii ipate Uhuru. Wengi watakuja kukumbuka walikuwa wapi na walifanya nini siku walipopata taarifa hizo za kutisha. Binafsi, taarifa ile ya mauaji ya Daud Mwangosi siku ile ya Jumapili ya huzuni kwa Taifa ilinikuta nikiwa Iringa Mjini. N umbali wa mwendo wa saa moja kwa gari kufika eneo la tukio, Nyololo, Mufindi.
Jioni ile nilikuwa nikifundisha soka ya watoto. Mara baada ya kupata taarifa zile kwa simu, nilisitisha mazoezi yale ya watoto. Nikawapa taarifa zile. Nilipowaambia kuwa nimepata taarifa sasa hivi kuwa mwandishi wa habari ameuawa Mafinga, mtoto mmoja akaniangalia na kuniuliza; “ Kwanini?”
Ndiyo, swali la mtoto yule ndilo umma wa Watanzania unapaswa uendelee kujiuliza hata leo; KWA NINI?
Mwandishi wa habari ni mjumbe katika jamii. Anapokuwa akifanya kazi yake hapaswi kuwa na hofu ya kudhuriwa kwa kukusudia na waliopata mafunzo ya kutumia silaha. Ndivyo ilivyo kwa watumishi wa Msalaba Mwekundu, wanapokuwa kazini kwenye maeneo hata ya vita.
Askari asiyejua kutofautisha kati ya mwanahabari aliyeshika kamera, mtu wa Msalaba Mwekundu aliyeshika mkoba wa Huduma ya Kwanza na raia anayefanya vurugu au adui aliyeshika silaha vitani, huyo hawezi kuwa ni askari makini.
Na hakika, kama Taifa, tunafanya makosa kuamini, kuwa nchi yetu ni ya amani kwa vile wananchi wetu hawagombani. Kama watu hawagombani kuwa na maana nchi ni ya amani yaweza kuwa tafsiri potofu ya maana nzima ya amani. Maana, kama watu hawagombani mahali pasipo na haki, usawa na uadilifu wa viongozi; mahali palipojaa dhuluma,unyanyasaji na maovu mengine wanayotendewa au wanaotendeana wanajamii, basi, amani hiyo itakuwa ni ya muda tu.
Maana, kwa watu wenye kuishi kwenye mazingira hayo bila kugombana wala kutokea uvunjifu wa amani, hiyo itakuwa na maana ifuatayo; ama watu hao hawaelewi kuwa wanaishi katika mazingira hayo ya dhuluma na maovu mengine wanayotendewa au kutendeana, au wamejawa na hofu.
Hivyo basi, kwa hilo la mwisho, itakuwa ni amani iliyojengeka katika misingi ya hofu. Na hofu hiyo haiwezi kuwa ya kudumu. Kuna siku mwanadamu hufikia ukomo wa kuhofia. Ukimwandama sana mjusi, mwisho hugeuka nyoka! Ndipo hapo tunapoona nchi zinalipuka na watu kuchinjana.
Hii ni nchi yetu. Katika tofauti zetu hizi za kiitikadi tusifike mahali tukashindwa kuongea kama Watanzania kwa kutanguliza maslahi ya Tanzania. Kuna umma uliopo na unaokuja. Umma unaotegemea sana busara katika uongozi wetu. Tuanze sasa kujenga utamaduni wa kuitumikia nchi yetu kwa kufanya na kuamua yale yenye maslahi kwa Tanzania. Hivi vyama vya siasa vipo leo na kesho havipo. Vinakuja na kuondoka, lakini Tanzania kama nchi itakuwapo daima.
Tusifike mahali tukabaki tunawaangalia wanasiasa wetu, kwa maslahi yao binafsi, ya makundi yao na vyama vyao, wakashinikiza au kuelekeza yale yenye kuchochea machafuko makubwa ya kijamii. Ni wajibu wa viongozi wa kisiasa kutanguliza busara katika kila maamuzi wayafanyao.
Na tunafanyaje pale tunapowaona viongozi wa kisiasa na watendaji wakifanya maamuzi yasiyo na busara na kusababisha Watanzania wenzetu kupoteza uhai na hata kuchochea machafuko?
Jibu; Kama Watanzania wazawa na wazalendo wa nchi hii, tuna wajibu wa kuyalaani matendo yao maovu.
Na katika nchi zetu hizi, ni kazi rahisi sana kuanzisha vurugu na kujenga mazingira ya chuki na uhasama, lakini, ni kazi kubwa sana kumaliza vurugu na kuondosha mazingira hayo ya chuki na uhasama. Na nchi yetu kamwe haiwezi kupiga hatua za maana za maendeleo katikati ya mazingira ya vurugu, chuki na uhasama, uwe wa vyama vya siasa au wanajamii.
Kihistoria, Watanzania tumeishi kwa amani na upendo bila kuwa na chuki na uhasama miongoni mwetu unaotokana na tofauti zetu za kidini na kikabila. Tunaziona sasa, dalili za baadhi ya wanasiasa, kwa malengo ya kisiasa, kutaka kupandikiza miongoni mwetu uhasama na chuki kwa kutumia tofauti zetu za kidini na kikabila, tofauti zetu za kiitikadi. Wanafanya hivyo mara ile wanaposhindwa kujenga hoja za kisiasa kwenye majukwaa ya kisiasa. Hawa ni watu hatari sana kwa maslahi ya taifa letu.
Katika nchi zetu hizi, ni wanasiasa wa aina hii ambao, katika kufanikisha malengo yao, huwa tayari hata kuwalipa vijana wasio na ajira na kuwavutisha bangi ili washiriki vurugu za kisiasa, kidini na kikabila. Tumeyaona hayo Liberia, Ivory Coast na hata katika nchi jirani na kwetu.
Tusipokuwa makini, yako karibu kupisha hodi kwenye nchi yetu, kama si tayari kuwa yameshaingia ndani ya nchi yetu.
Hii ni nchi yetu. Tutafanya makosa makubwa kuwaachia viongozi wa kisiasa pekee, jukumu la kulinda maslahi ya nchi yetu. Tunapita sasa katika kipindi kigumu tangu tupate Uhuru. Dunia imebadilika, na nchi yetu inapitia kwenye kipindi cha mabadiliko. Hakuna mtu au chama cha siasa kinachoweza kuyazuia mabadiliko haya. Kufanya hivyo ni kutuletea machafuko na kuvunja amani yetu. Tuna jukumu la kufanya tunayoweza, na kwa kutanguliza busara, kuipitisha salama nchi yetu katika kipindi hiki cha mabadiliko.
Maana, tukiingia kwenye machafuko, basi, hakutakuwa na mshindi, maana, sote tutashindwa. Na kifo cha Daudi Mwangosi kinatutaka tuyatafakari haya.
source:http://mjengwablog.com/
No comments:
Post a Comment