(picha kwa hisani ya ITV)
Baadhi ya wakazi wa eneo la Mivinjeni Kurasini jijini Dar es Salaam wamefunga barabara ya Kilwa kwa saa kadhaa huku wakiwasha moto katikati ya barabara hali iliyosababisha msongamano wa magari baada ya kutangaziwa kuwa nyumba zao zinabomolewa hivyo waondoke ili kupisha mradi.
......SOMA ZAIDI....
Katika sakata hilo ITV imeshuhudia baadhi ya wananchi wakiwa wamelala barabarani na wengine wakichoma matairi katikati ya barabara ambapo wamedai kuwa wameamua kufanya hivyo ili kuishinikiza serikali isitishe zoezi la kuwabomolea nyumba zao hadi itakapowalipa haki zao zote na kuwaonyesha maeneo mengine ya kuhamia.
Hata hivyo kabla askari wa kikosi cha kutuliza ghasia kuwasili eneo hilo awali walitanguliwa na askari wa kawaida ambao walionekana kuwatuliza watu hao kwa kuwataka kuondoa mawe walioweka barabarani bila mafanikio na ndipo askari kanzu ambaye jina lake halikufahamika mara moja alipoingilia kati na kuwaomba wananchi hao watulie ili watumiaji wa barabara hiyo waweze kuendelea na safari zao na kuwaahidi kushirikiana nao kufuatilia suala hilo.
Baada ya heka heka hizo kutulia gari la zimamoto liliwasili eneo hilo na kufanikiwa kuzima moto ambao bado ulikuwa unaendelea kuwaka na ITV ilifika katika ofisi za mwenyekiti wa serikali za mtaa ambaye anadaiwa kutoa tangazo hilo ili kupata ufafanuzi juu ya suala hilo bila mafanikio baada ya kukuta ofisi yake ikiwa imefungwa.
Mgogoro huo kati ya serikali na wananchi wa Mivinjeni eneo la Kurasini umedumu kwa zaidi ya miaka kumi sasa ambapo wanatakiwa kuondoka ili kupisha mradi waliodai kuwa hawaujui.
No comments:
Post a Comment