Shahidi wa 10 katika kesi ya usafirishaji wanyama hai nje ya nchi
amemtaja mshitakiwa wa kwanza, Kamran Mohamed, ambaye ni raia wa
Pakistan kuwa alimzawadia Sh. 120,000 kwa ajili ya kazi aliyoifanya ya
kupakia wanyama hao kwenye ndege ya Qatar Airforce Novemba 25, 2010.
....SOMA ZAIDI....Akitoa ushahidi wake mbele ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Kilimanjaro,
Simon Kobelo, shahidi huyo ambaye ni mfanyakazi wa Kampuni ya Swissport
International inayohudumia mizigo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Kilimanjaro (KIA), Ally Mzava, alidai mahakamani kuwa siku hiyo alipewa
taarifa kuwa kutakuwa na ndege ya dharura.
Kwamba, ndege hiyo itafika KIA usiku na kupakia ndege, hivyo
alitakiwa kuwataarifu wenzake ili wawe tayari kwa ajili ya kupakia
wanyama hao.
Mzava alidai kuwa mara baada ya kupewa taarifa hiyo kutoka kwa mkuu
wa kitengo cha ndege za dharura aliyemtaja kwa jina la Rosemary Michael,
aliwaandaa wenzake na baada ya ndege hiyo kufika KIA, walianza kupakia
mizigo hiyo, ambayo ilikuwa imefungwa kwenye maboksi.
“Tuliifanya kazi hiyo kwa umakini. Tukiwa ndani ya ile ndege pale
pale uwanjani, nilipewa Sh. 120,000 kama ‘tip’ (bakshishi) ya kazi
tuliyoifanya na kuambiwa na Mhindi aliyekuwamo mle ndani kuwa nigawane
na wenzangu…ninamfahamu ni yule Mhindi pale nasikia wanamwita Kamran,”
shahidi huyo aliiambia mahakama.
Alidai baada ya kumaliza kazi hiyo, aliondoka na hakujua kilichoendelea kutokana na kazi aliyotakiwa kuifanya kukamilika.
Shahidi huyo alidai ndege hiyo ilikuwa imeandikwa ubavuni jina la Qatar Airforce One.
Shahidi mwingine, Joseph Mpimbwe, ambaye ni msimamizi katika Kampuni
ya Swissport iliyopewa dhamana ya kupakia na kushusha mizigo kwenye
ndege KIA, alidai aliona twiga wawili wakipakiwa kwenye ndege.
Mbele ya Hakimu Kobelo, shahidi huyo alidai katika tarehe hiyo
alipigiwa simu na Rosemary na kupewa taarifa ya kuwapo kwa ndege
itakayosafirisha wanyama usiku wa manane. Alidai kuwa baada ya kupigiwa
simu hiyo, alimpigia simu Moris Njau na kumpa taarifa hiyo ili awaandae
wafanyakazi wenzake kwa ajili ya upakiaji wa wanyama hao.
“Nilipata bahati ya kuona twiga wawili wakiwa wamefungwa kwenye boksi
na kulikuwa na vifurushi vingi vilivyokuwa vimefungwa. Siyo mara ya
kwanza kupakiza wanyama,” aliiambia mahakama na kuongeza:
“Na tumekuwa tukifanya hivi mara kwa mara, ndege iliondoka kesho yake
asubuhi baada ya sisi kumaliza kupakia wanyama hao. Ilikuwa saa 12:00
kasoro,” alidai.
Hata hivyo, shahidi huyo alidai hawawezi kupakia mzigo kwenye ndege
bila ya kuwa na kibali kinachoeleza aina ya mzigo, uzito wake na
anayehusika nao (cargo manifest), ambayo inaelezea aina ya mzigo
unaopaswa kupakiwa au kushushwa kwenye ndege.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Septemba 24, mwaka huu mashahidi wengine watakapoendelea kutoa ushahidi wao.
Wanyama hao wanadaiwa kutoroshwa kwa kutumia ndege ya Quatar Emiri
Air Force kwenda Doha, nchini Qatar, Falme za Kiarabu kupitia KIA.
Inadaiwa kuwa wanyama aina tofauti 144 na ndege pori wawili.
Katika orodha hiyo, inadaiwa kuwa kulikuwa na twiga na viroba vya nyama pori ya kukausha zaidi ya tani tano.
Utoroshaji huo unadaiwa kuwa uliikosesha serikali zaidi ya Sh.
milioni 170. Ilidaiwa kuwa wanyama hao walipakiwa usiku wa manane
Novemba 24, 2010 na kuwa kampuni ya uwindaji wanyama ya Ham Marketing na
Kampuni ya Uwindaji Ndege ya Luwego Bird Trappers ndizo zilizokamata
wanyama hao na ndege.
No comments:
Post a Comment