Kiungo/winga
wa muda mrefu wa klabu ya Manchester United Ryan Giggs ameteuliwa kuwa
kocha mchezaji ndani ya klabu hiyo ambapo atakuwa akisaidiana na kocha
David Moyes pamoja na makocha wengine wasaidizi .
Mchezaji huyo ambaye amekuwa na United kwa misimu 23 akiwa ameichezea
klabu hiyo tangu akiwa na umri wa miaka 14 amekuwa akisomea ukocha kwa
muda mrefu ambapo tayari amepata shahada mbalimbali za UEFA huku akiwa
anamalizia shahada yake ya mwisho ambayo ni UEFA Pro License .
Giggs akiwa na umri wa miaka 40 ni mchezaji mwenye umri mkubwa kuliko
wote ndani ya United na ana rekodi ya kuwa mchezaji pekee aliyefunga
mabao kwenye kila msimu wa Ligi kuu ya England tangu ilipoanzishwa mwaka
92 na uteuzi wake unamaanisha kuwa atakuwa akifanya kazi yake kwenye
kikosi cha kwanza cha timu hiyo huku akibakia kuwa mhezaji baada ya
kusaini nyongeza ya mkataba wa mwaka mmoja mwezi wa nne mwaka huu.
Akiwa amecheza zaidi ya 1000 za United kwenye kiwango cha juu uzoefu
wa Giggs utakuwa silaha muhimu kwa kocha mpya David Moyes ambaye ndio
kwanza ameanza kazi ya kuifundisha United Jumatatu ya wiki hii akiwa
ameteuliwa kuchukua nafasi ya Sir Alex Fergusson aliyestaafu baada ya
msimu uliopita akiwa amekaa kwenye benchi la United kwa miaka 26 .
Uteuzi huu unaweza kuwa mwanzo wa maisha mapya ya Giggs kwenye tasnia
ya ukocha pale atakapoamua kustaafu kucheza soka kwani amekuwa
akisomea ukocha kwa muda mrefu na tayari ana vyeti vya kutosha na nafasi
hii mpya itamuongezea uzoefu ambao utamfanya kuwa moja ya mahaguo ya
kwanza kurithi nafasi ya David Moyes pale atakapofikia mwisho wake kama
kocha .
Zaidi ya Giggs mchezaji wa zamani wa United ambaye alikuwa nahodha wa
Everton wakati David Moyes akiwa kocha mkuu Phil Neville anatarajiwa
kujiunga na benchi la ufundi la United baada ya kutangaza kustaafu
kucheza soka msimu uliopita.
Neville naye ana uzoefu wa ukocha akiwa amewahi kufanya kazi kama
mmoja wa makocha wasaidizi wa timu ya taifa ya England kwa wachezaji
wenye umri chini ya miaka 21 na kama Giggs amekuwa akisomea kozi kadhaa
za ukocha ambazo amefuzu akiwa anashikilia shahada za UEFA B na UEFA A .
Neville mwenye umri wa miaka 36 aliichezea United kwa muda wa miaka 10
tangu mwaka 1995 mpaka 2005 ambapo alicheza mechi 263 kabla ya kuhamia
Everton alikocheza kwa miaka 10 alipocheza mechi 242 kabla ya kustaafu
mwishoni mwa msimu uliopita .
No comments:
Post a Comment