facebook likes

Sunday, February 10, 2013

MSAKO WA WALIOFICHA FEDHA NJE YA NCHI WAANZA

Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Serikali imeunda Kamati maalumu ya kitaifa kuchunguza na kubaini majina ya Watanzania wanaodaiwa kuficha fedha nje ya nchi kinyume na sheria na kanuni za nchi.

Pamoja na kuchunguza, Kamati hiyo yenye wajumbe wanane iliyoundwa Januari 9, itachunguza iwapo fedha hizo ni haramu au la.

Hayo yalisemwa bungeni jana na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alipokuwa anatoa hoja ya kuahirisha Mkutano wa 10 wa Bunge mjini hapa.

Hatua ya kuundwa Kamati hiyo ilitokana na Azimio namba 9/2012 likiitaka Serikali kuchukua hatua dhidi ya Watanzania hao. Azimio hilo lilizaliwa na hoja binafsi ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto. 

Kwa mujibu wa Azimio hilo, Serikali inatakiwa kuwasiliana na Benki ya Dunia kupitia kitengo cha urejeshaji mali, ili mabilioni yanayomilikiwa na Watanzania katika benki za nje ambako hufichwa kwa kukwepa kodi, yarudishwe nchini.

Lakini pia Watanzania wote wenye akaunti za fedha nje ya nchi waeleze wamezipataje ili Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ichukue hatua za kisheria dhidi ya wamiliki wa fedha na mali kinyume na mapato yao halali. 

Serikali ilikubali, kwamba katika Mkutano wa Bunge wa 11 itawasilisha taarifa ya hatua iliyochukuliwa ili kuziba mianya ya utoroshaji wa fedha nje ya nchi.

Mbali na kuchunguza uhalali wa fedha hizo, Kamati hiyo ambayo wajumbe wake hawajatajwa kwa majina, pia itatakiwa kutambua benki na nchi zilikofichwa fedha hizo na pia kuandaa mashitaka dhidi ya Watanzania watakaobainika kuficha fedha haramu nje ya nchi; na kuishauri Serikali jinsi ya kuzuia uhalifu wa makosa ya fedha.

“Ili kuiwezesha Kamati hii kufanya kazi yake kwa ufanisi, ni wazi kwamba itahitaji ushirikiano mkubwa kutoka kwa wananchi kwa kutoa taarifa kuhusu suala hili. Hivyo, wananchi wote wenye taarifa sahihi na za ukweli zinazoweza kuisaidia Kamati kutekeleza kazi hii, wajitokeze kutoa maoni yao kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kushirikiana kwa karibu na Kamati …waheshimiwa wabunge nao nawaomba kutoa ushirikiano wa kufanikisha kazi za Kamati hii,” alisema Waziri Mkuu.

Kuhusu hali ya amani nchini, Waziri Mkuu alielezea kuwapo hivi karibuni dalili za kupoteza sifa ya umoja wa kitaifa na amani ambavyo vimedumu kwa miaka mingi, kwa wananchi kushuhudiwa wakishindwa kuvumiliana, japo kwa tatizo dogo tu miongoni mwao. 

Vyama vya siasa vimeonesha dalili ya kuhamasisha wanachama kuingia kwenye malumbano ya siasa  baina  yao  wenyewe  kwa  wenyewe au baina ya chama  na kingine na baadhi ya wanachama kushikana mashati na kujeruhiana. 

“Napenda kutumia fursa hii, kuasa viongozi wa vyama vya siasa kuepuka kutumia majukwaa ya siasa kuvuruga amani na utulivu uliopo. Waepuke matamko ya vitisho na kuhamasisha wanachama kuendeleza vitendo vya uvunjifu wa amani na kujenga chuki na uhasama miongoni mwa jamii na kwa Serikali halali iliyoko madarakani,” alisema Pinda.  

Aliongeza kuwa pamoja na kutofautiana kwa mawazo na sera za vyama vya siasa, ni muhimu kujenga mazingira ya kuvumiliana kwa hali ya juu katika kujenga demokrasia ya kweli nchini. 

“Viongozi wa vyama wanatakiwa kueleza sera zao badala ya kutukanana, kubezana, kushutumiana na kuzomeana. Tujenge nchi yetu kwa amani na utulivu ndipo tutapata maendeleo endelevu,” aliasa.

Alisema kumeibuka pia chokochoko za kidini; baadhi ya waumini wa dini wamekuwa wakikashifu dini nyingine kwa kejeli na vitendo vingine visivyostahili, ambapo pia baadhi ya viongozi wa madhehebu ya dini wamekuwa wakiwaingiza waumini wao katika migogoro isiyokwisha, ikiwa ni pamoja na kufungiana milango na kuzuia waumini kuabudu siku za ibada. 

“Napenda kusisitiza, kuwa madhehebu ya dini yana nafasi kubwa ya kujenga umoja wa kitaifa, amani na mshikamano. Nawaomba viongozi wa madhehebu ya dini kutatua kwa amani migogoro iliyopo na kuelimisha waumini wao kuthamini, kujenga na kuenzi amani na utulivu uliopo. 

“Serikali imetoa uhuru wa wananchi kuabudu, kila mtu kwa dini anayoitaka. Hivyo, hakuna sababu ya dini moja kukashifu nyingine. Aidha, tupinge kwa nguvu zetu zote chokochoko za kidini ambazo zimeanza kujitokeza sehemu mbalimbali nchini,” alisema.
Aliyagusa pia mashirika yasiyo ya serikali (NGOs) akisema baadhi yao yamekuwa yakihusishwa kuwa mstari wa mbele kurubuni wananchi kufanya vurugu zinazolenga uvunjifu wa amani wakati yana jukumu kubwa la kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kujenga umoja wa kitaifa. 

“Viongozi wa mashirika haya waepuke kutumiwa na baadhi ya viongozi, kupanda mbegu mbaya kwa wananchi kuvuruga amani,” alisema.

Kwa upande wa vyombo vya habari, alisema kumekuwa na kutiliana shaka kwa baadhi ya vyombo hivyo kuandika habari za uchochezi, hivyo kuashiria uvunjifu wa amani na mshikamano wa kitaifa. 

“Vyombo vya habari vina wajibu mkubwa wa kuelimisha umma na kuhabarisha kuhusu masuala ya maendeleo, kama wafanyavyo jirani, hususan vyombo vya habari vya Rwanda. Aidha, vyombo hivi vina fursa nzuri ya kutumia uhuru uliopo kudumisha amani na utulivu nchini,” alisema.

Kuhusu nini kifanyike, Waziri Mkuu aliitaka Serikali, wananchi na wadau wote vikiwamo vyama vya siasa, madhehebu ya dini, vyombo vya habari, mashirika yasiyo ya serikali, n.k. wakae wazungumze na kutafakari kuhusu hali hiyo.

“Tunapaswa kwa namna zote tuvumiliane na kuheshimiana kwa kuzingatia utamaduni wa kitanzania na misingi ya amani na utulivu tuliojijengea kwa muda mrefu; na wananchi wote tuzingatie na kuheshimu utawala bora wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo,” alishauri Waziri Mkuu.

Akizungumzia hali ya chakula nchini, Waziri Mkuu alisema tathmini iliyofanyika hivi karibuni juu ya chakula na athari za mvua zinazoendelea kunyesha, inaonesha kuwa maeneo mengi hasa  yanayopata mvua za msimu, ya Mbeya, Ruvuma, Rukwa, Iringa, Tabora na Mtwara, mazao mengi yako katika hatua mbalimbali za ukuaji na kama mvua zitaendelea vema, upatikanaji wa chakula katika maeneo hayo utakuwa mzuri.

Hata hivyo, alisema kuna upungufu wa chakula katika wilaya 47 katika mikoa 15 ambazo zitahitaji msaada wa chakula katika vipindi tofauti ambapo inakadiriwa kuwa jumla ya watu 1,615,445 watahitaji jumla ya tani 32,870 za chakula. 

“Kutokana na matarajio hayo ya uhaba wa chakula, Serikali itahakikisha Kitengo cha Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA) kinaendelea kusambaza mahindi katika maeneo yenye uhaba. Hadi sasa jumla ya tani 20,000 zilishatolewa kwa mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Dodoma, Singida, Morogoro, Lindi, Tanga, Mtwara, Pwani, Dar es Salaam, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara na Tabora,” alisema. Bunge liliahirishwa hadi Aprili 9, Dodoma.

No comments:

COMMENTS

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...