KAMPUNI ya ujenzi na uhandisi wa
majengo ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC)
imesema iko tayari kuja Tanzania na kujenga upya reli ya kati ili iwe ya
kisasa zaidi endapo wataombwa wafanye hivyo.
Hayo yamesemwa jana jioni (Ijumaa,
Oktoba 18, 2013) na Rais wa CCECC, Bw. Yuan Li alipofanya mazungumzo na
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda jijini Beijing, China. Waziri Mkuu jana
alikuwa katika siku ya tatu ya ziara yake ya kikazi ya siku tisa kwa
mwaliko wa Serikali ya nchi hiyo.
Akizungumza na Bw. Li pamoja na baadhi
ya viongozi kutoka Tanzania alioambatana nao, Waziri Mkuu alimweleza
Bw. Li kwamba hivi sasa reli hiyo imechakaa hali inayofanya mizigo mingi
kutoka bandarini isafirishwe kwa barabara na hivyo kuongeza gharama kwa
wasafirishaji.
Alisema hali hiyo inachangia mzigo kwa
Serikali kwani kumekuwa na uharibifu mkubwa wa barabara kutokana na
uzito wa magari yanayobeba mizigo kutoka bandari ya Dar es Salaam hadi
nchi jirani kwa sababu wanaitegemea sana bandari hiyo kwa kupokelea
mizigo.
Alipoulizwa ni uzito kiasi gani
unaruhusiwa kwenye barabara za nchini China, Bw. Li alijibu ni tani 25
(axle load) hali iliyomshtua Waziri Mkuu ambaye alilazimiak kumweleza
mgeni wake kwamba barabara za Tanzania haziwezi kudumu kwa miaka mingi
kwani hivi sasa zinaruhusu magari yenye uzito wa tani 56 kupita kwenye
barabara zake.
Alisema kutokuwepo kwa usafiri
madhubuti wa reli imekuwa ni kikwazo kikubwa cha usafiri kati ya Dar es
Salaam na Kigoma na Tabora hadi Mwanza lakni pia kutoka Tabora hadi
Mpanda. "Kukamilika kwa reli hii ambayo ni uti wa mgongo wa Taifa letu,
kutasaidia hapo baadaye kufungua milango na Burundi, Rwanda na DRC
lakini pia tutaweza kupeleka mizigo hadi Uganda kwa kupitia Mwanza,"
alifafanua.
Kwa upande wake, Bw. Li alimweleza
Waziri Mkuu kuwa tayari wameanza mazungumzo na Wizara ya Uchukuzi na
iwapo watafikia muafaka wako tayari kuja kuijenga reli hiyo.
Akitoa mfano wa zoezi kama hilo, Bw.
Li alisema kutokana na mkopo wa benki ya Exim ya China, Septemba mwaka
huu, wameanza ujenzi wa reli kati ya Djibouti na Sudan Kusini pamoja na
reli nyingine ya kuunganisha Djibouti na Ethiopia ambapo zote mbili
zinatarajiwa kukamilika baada ya miaka miwili.
"Hatuwezi kufumua reli yote kwa mara
moja. Ninachoona hapa, ujenzi wake itabidi uende kwa awamu kwa sababu
una gharama kubwa lakini kwa kuanzia tunaweza kuanza Dar es Salaam hadi
Morogoro, awamu ya pili tukatoka Morogoro hadi Dodoma na kuendelea ili
usafiri wa treni uwe ukiendelea wakati ujenzi wa reli nao ukiendelea,"
alishauri.
Kampuni ya CCECC ndiyo iliyojenga reli
ya Tanzania hadi Zambia (TAZARA) yenye urefu wa kilometa 1,860 na
madaraja 320. Ujenzi wake ulianza mwaka 1970 na kukamilika mwaka 1976.
Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu
amefuatana na Waziri wa Nchi, (OWM) Uwezeshaji na Uwekezaji, Dk. Mary
Nagu; Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda; Waziri wa
Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe; Waziri wa Uvuvi na Mifugo wa Zanzibar,
Bw. Abdallah Jihad Hassan; Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa, Bw. Mahadhi Juma Maalim na Naibu Waziri wa Fedha, Bibi
Saada Salum Mkuya.
Pia amefuatana na Balozi wa China,
Luteni Jenerali (Mst.) Abdulrahaman Shimbo, Wakuu wa mikoa ya Mtwara,
Shinyanga na Simiyu; wabunge wawili, Bw. Godfrey Zambi (Mbozi) na Dk.
Titus Kamani (Busega) na viongozi wakuu wa Tanzania Private Sector
Foundation, Bw. Reginald Mengi, Bw. Salum Shamte na Bw. Godfery Simbeye.
No comments:
Post a Comment