SOMA ZAIDI........
Kwa mujibu wa taarifa za uhakika kutoka ndani ya kikao cha Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kilichomalizika hivi karibuni Arusha, ushuru huo ulianza kutozwa rasmi kwa magari hayo juzi.
Hali hiyo imesababisha mtafaruku katika eneo la Rusumo, mpakani mwa Tanzania na Rwanda, ambako zaidi ya malori 200 yenye mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam, yamekwama kwa kushindwa kulipa kiwango hicho kipya cha ushuru wa barabara.
Awali nchi hiyo ilikuwa ikitoza ushuru wa dola za Marekani 16 kwa kila kilometa 100, ushuru ambao ndio uliokuwa ukitozwa na Tanzania kwa malori yaliyokuwa yakipitisha mizigo kwenda nchi za nje.
Hata hivyo, katika kilichoonekana kuwa mazingira yasiyo sawa ya kupata faida kutokana na udogo wa eneo wa nchi hiyo, Rwanda iliamua kupandisha ushuru huo, kutoka dola 16 kwa kilometa 100, hadi dola 152 bila kuzingatia kilometa.
Kabla ya kupandishwa kwa ushuru huo, Tanzania ilionekana kupata faida, kwa kuwa kutoka Dar es Salaam hadi Rusumo, ni kilometa 1,350 na hivyo kwa ushuru wa dola 16 kwa kilometa 100, Serikali ilipata dola 216 kwa gari.
Kwa Rwanda taarifa zinaeleza kuwa hali ilikuwa tofauti kutokana na udogo wa nchi, ambapo kutoka Rusumo hadi Kigali ni kilometa 139, ambao kwa ushuru huo wa dola 16 kwa kilometa 100, Serikali ya Rwanda ilijikuta ikiambulia dola 22.24 tu kwa gari.
Kutokana na mazingira yaliyoonekana ya kutopata sawa na Tanzania, yaliyotokana na udogo wa nchi husika, Rwanda ilipandisha ushuru huo na kuwa dola 152 bila kujali umbali, kwa kuwa kijiografia haukuwa na msaada kwao.
Hata hivyo, taarifa zimeeleza kuwa Tanzania haikulalamika kwa ongezeko hilo la ushuru na iliendelea kufanya biashara na Rwanda kama inavyofanya na nchi zingine zinazopitisha mizigo yao katika Bandari ya Dar es Salaam.
Hujuma kwa Tanzania
Katika mazingira yanayotafsiriwa kuhujumu Bandari ya Dar es Salaam, nchi hiyo mwanachama mwenza wa Afrika Mashariki, imepandisha ushuru tena hadi dola 500, mara hii ushuru huo ukiwa kwa magari yanayopita Bandari ya Dar es Salaam tu.
Ushuru huo kwa mujibu wa taarifa hiyo, ulitangazwa ghafla muda mfupi baada ya Kenya kutangaza kuondoa vikwazo vya barabara kwa magari ya mizigo inayopita katika Bandari ya Mombasa kwenda Kigali.
Mfanyabiashara aliyeathirika na ushuru huo, alisema sasa ni wazi kuna jaribio la Rwanda kuonesha kuwa usafirishaji wa mizigo kutoka Dar es Salaam kwenda Kigali, umbali wa kilometa 1,350, ni aghali kuliko kusafirisha mizigo kutoka Bandari ya Mombasa hadi Kigali, umbali wa zaidi ya kilometa 2,700.
Taarifa rasmi
Akizungumza na gazeti hili jana, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tizeba, alikiri Wizara yake kupata taarifa za kupanda kwa ushuru huo kupitia wafanyabiashara, lakini hadi sasa wizara hiyo haijapewa taarifa rasmi na Rwanda.
Alisema juzi akiwa katika kikao hicho cha mawaziri wa Afrika Mashariki, Wanyarwanda walikuwa wakilalamikia kiasi cha ushuru kinachotozwa nchini katika barabara kuwa ni mkubwa ikilinganishwa na nchi za Afrika Mashariki.
Alisema kutokana na malalamiko hayo, alilazimika kuwajibu kuwa ushuru huo ni lazima utozwe kutokana na vigezo vilivyowekwa na lengo lake kubwa ni kulinda barabara.
“Kama Wizara hatujapata taarifa rasmi, lakini tumepokea malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara kuhusu kutozwa ushuru huo mpya, tunachofanya sasa ni kuangalia namna suala hili litakavyoathiri usafirishaji na baada ya hapa, tutashauri wizara za fedha na ujenzi hatua za kuchukua,” alisisitiza.
Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax ambaye sasa ni Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), alisema hatua hiyo ya Rwanda kupandisha ushuru ni ya kutengeneza ushindani usio sawa.
Kwa mujibu wa Dk Tax, kwa sasa Bandari ya Dar es Salaam inafanya vizuri ikilinganishwa na ya Mombasa na ndiyo maana anaona ushuru huo ni wa kuweka mazingira yasiyo sawa ya ushindani kati ya Bandari ya Dar es Salaam na ya Mombasa.
“Tangu Rwanda ilipojiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki, ilikuwa ikilalamikia vikwazo vya Tanzania vya barabara, lakini ukweli ni kwamba Tanzania na Kenya zimekuwa zikijenga barabara zake zenyewe, ndiyo maana ni vema zitengeneze mkakati wa kudhibiti matumizi ya barabara hizo ili zikiharibika kuwe na fedha za kuzikarabati,” alisema.
Suluhisho
Hata hivyo, Dk Tax alisisitiza kuwa kabla ya kuondoka wizara hiyo ya Afrika Mashariki, tayari nchi za Jumuiya hiyo zilikuwa na mkakati wa kuanza kutumia kiwango kimoja cha uzito wa magari kisichozidi tani 55, ili kuhakikisha miundombinu ya nchi hizo hususani barabara haiharibiwi na uzito wa magari hayo.
“Hili ndilo suluhisho la pekee iwapo nchi zote za Afrika Mashariki zitakuwa na kiwango kimoja cha uzito, hata tozo za ushuru zitakuwa sawa na ushindani inaowaumiza wafanyabiashara hautakuwapo,” alisisitiza.
Msemaji wa Chama cha Umoja wa Wasafirishaji wa Malori nchini (TATOA), Zacharia Hans-Pope, alikiri kuwa na taarifa za kupandishwa kwa ushuru huo na hadi jana jioni magari ya mizigo zaidi ya 200 yalikuwa yamekwama Rusumo kutokana na kushindwa kulipa tozo hiyo.
“Magari zaidi ya 200 yamekwama pale Rusumo kwa kuwa hayana uwezo wa kulipa tozo hiyo… ni kubwa mno, sisi chama tunasubiri tamko la Serikali ya Tanzania, kwanza hatukuwa na taarifa kabisa juu ya suala hili,” alisisitiza.
Alisema ushuru huo utakuwa ‘mwiba’ kwa Bandari ya Dar es Salaam kwa kuwa utaifanya ionekane kuwa ya gharama kusafirisha mizigo kwenda Kigali jambo ambalo si la kweli.
Ni nchi za SADC pekee ndizo zenye ushuru mmoja wa barabara ambao ni dola 16 kwa kilometa 100 za barabara, lakini bado Jumuiya ya Afrika Mashariki haijaweka kiwango kimoja cha tozo hiyo.
source:alvincollections
No comments:
Post a Comment