SAKATA la kodi ya simu ya Sh 1,000 kwa
kila laini ya simu kwa mwezi, inayolipwa na watumiaji wa simu,
litamalizwa bungeni kisheria.
Waziri wa Fedha, William Mgimwa, amesema
wameanza kutekeleza agizo la Rais Jakaya Kikwete, la kuitaka Wizara ya
Fedha kukutana na wadau wengine, kuangalia namna ya kupata vyanzo
vingine vya mapato mbadala wa kodi hiyo.
Alisema hayo alipozungumza jana na Habari leo, baada ya kusaini mkataba wa msaada wa zaidi ya Sh bilioni
344, kutoka Benki ya Dunia, ili isaidie masuala mbalimbali katika sekta
ya usafirishaji.
Mgimwa alisema katika suala hilo, masuala ya kisheria
yatafikishwa bungeni mwezi ujao, ili kumaliza utata wa kodi hiyo.
Alisema uamuzi wa kushughulikia suala
hilo, ulifikiwa kutokana na agizo la Rais Kikwete la hivi karibuni,
kutaka wizara hiyo na ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia kukaa na
kampuni za simu kumaliza utata uliojitokeza kuhusu kodi hiyo.
Awali Umoja wa Wamiliki wa Kampuni za
Simu (MOAT), ulitoa maoni kutaka kufutwa kwa kodi hiyo, kutokana na
kulalamikiwa na wadau wa sekta ya mawasiliano.
Mbali na Moat, pia baadhi ya viongozi wa
Serikali, wabunge na wananchi, walipinga kodi hiyo kwa walichokieleza
kuwa itaongeza mzigo wa ugumu wa maisha kwa mtumiaji, hususan wa kipato
cha chini.
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari
Makamba, alipozungumza na gazeti hili jana, alisema mara baada ya Rais
kutoa agizo, wizara husika zilikutana kufanyia kazi agizo hilo.
"Rais akishaagiza kinachofuata ni
utekelezaji na sisi kesho yake tulianza vikao na ninachoweza kukwambia
tuko pazuri na tukikamilisha majadiliano yetu, tutatoa taarifa," alisema
Makamba.
Alisema lengo ni kuangalia kama Serikali
inaweza kupata Sh bilioni 178 kutoka vyanzo vingine, iwapo itaamua
kufuta kodi inayotokana na tozo ya Sh 1,000 kutoka kwenye laini za simu.
Hivi karibuni, Rais Kikwete aliagiza
Wizara za Serikali zinahusika na kodi na mawasiliano na kampuni za simu
za mikononi nchini, kukutana kutafuta jinsi ya kumaliza mvutano wa kodi
hiyo.
Alitoa maelekezo hayo baada ya kukutana
na viongozi wa Wizara ya Fedha, Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia na wawakilishi wa kampuni za simu za TTCL, Airtel, Vodacom,
Tigo na Zantel.
Rais alisema lengo kuu la mkutano huo, liwe kupendekeza
jinsi ya kuziba pengo la Sh bilioni 178 ambazo zitapotea katika bajeti,
iwapo kodi hiyo itafutwa na Serikali kupitia marekebisho kwenye Muswada
wa Fedha wa Bajeti ya Mwaka 2013/14.
Aliwaambia wawakilishi wa pande hizo
mbili kuwa hawezi kuifuta moja kwa moja kodi hiyo, bila kutafuta njia
nyingine za kupata fedha za kujaza pengo litakalotokeza, huku tayari
Bunge limezipangia matumizi.
“Nakuombeni kaeni pamoja, wekeni bongo
zenu pamoja, wekeni akili yenu pamoja tutafute namna gani tutajaza pengo
hili la Sh bilioni 178, endapo tutakubaliana kuwa kodi hii inawabebesha
wananchi mzigo mzito na kuwa pengine menejimenti ya kodi yenyewe ni
ngumu,” alisema Rais Kikwete.
SOURCE: Habari Leo
No comments:
Post a Comment