Star wa timu ya taifa ya Senegal na klabu ya Newcastle United ya ligi kuu ya England Demba Pappis Cisse hatimaye ameonekana kusalimu amri na kukubali kuvaa jezi ya Newcastle ambayo itakuwa na nembo ya mdhamini mkuu wa Klabu hiyo ambaye ni kampuni ya Wonga.
Cisse ambaye ni nahodha wa timu ya taifa ya Senegal amekubali kuvaa jezi hiyo baada ya kugoma kutokana na sababu za imani ya dini yake ya uislamu ambayo haiafiki masuala ya riba kwenye mikopo au biashara, na ilifikia hatua ya kupewa adhabu ya kufanya mazoezi mwenyewe na kuachwa na klabu hiyo wakati wenzie walipoenda nchini Ureno kufanya mazoezi ya kabla ya msimu ambapo ilidhaniwa kuwa nyota huyo angeweza hata kufukuzwa kutokana na msimamo wake.
Siku chache zilizopita wadakuzi wa magazeti ya England walimnasa Cisse akiwa ndani ya Casino akiwa amekaa kwenye meza ya kucheza kamari jambo ambalo liwafanya watu washindwe kuelewa nini kinaendelea kwani kamari kama ilivyo kwa masuala ya riba ni haramu kwa Waislamu.
Wonga ni kampuni ambayo inafanya biashara ya kukopesha watu ambapo mikopo inayotolewa na kampuni hiyo inalipwa kwa kutoza riba ya juu jambo ambalo Cisse kama muumini safi wa dini ya kiislamu anapingana nalo.
Hata hivyo suala hilo limemalizwa baada ya Pande zote kukaa chini na kuzungumza na kupata ufumbuzi kwenye Kikao kilichoongozwa na viongozi wa chama cha wachezaji wa kulipwa nchini England PFA na sasa Cisse atavaa jezi za Wonga kama mchezaji mwingine yeyote wa Newcastle.
No comments:
Post a Comment