facebook likes

Tuesday, June 25, 2013

Wabunge Waridhia Bajeti ya Serikali

Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa akijibu hoja za wabunge waliochangia mjadala wa kupitisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 201314, Dodoma jana.

BUNGE limepitisha Bajeti ya Serikali ya Sh18.2 trilioni iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa katika Bunge la Bajeti linaloisha mwishoni mwa wiki hii. Wabunge 235 walipiga kura ya ndiyo kupitisha bajeti hiyo jana jioni baada ya Dk Mgimwa na manaibu wake wawili kumaliza kujibu hoja mbalimbali za wabunge kuhusu bajeti hiyo.
Akitaja majibu ya kura zilizopigwa kupitisha bajeti hiyo, Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel alisema wabunge wote wako 354 kati ya hao wabunge 83 hawakuwepo na kwamba waliopiga kura ni wabunge 270. Alisema 35 walisema hapana na 235 walisema ndiyo.
“Kwa mujibu wa kanuni zetu wabunge waliosema ndiyo wamezidi asilimia 50 ya adadi inayohitajika hivyo bajeti kuu imepitishwa rasmi,” alisema Joel.
Kati ya wabunge 83 ambao hawakuwepo wakati wa zoezi hilo la kupiga kura likifanyika wapo mawaziri sita. Mbunge wa Bariadi Mashariki(UDP), John Cheyo alipiga kura ya ndiyo na kufanya wabunge wa CCM wamshangilie kwa kufanya hivyo.
Kwa upande mwingine, wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, jana walisusia kikao cha Bunge cha kupitisha Bajeti ya Kuu, huku wakitoa sababu tano, ikiwemo shambulio la bomu katika mkutano wa chama hicho jijini Arusha.
Mbali na kususia kikao hicho, jana asubuhi Kiongozi wa Kambi hiyo, Freeman Mbowe, Mnadhimu Mkuu, Tundu Lissu, Mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema na Mbunge wa Nyamagana, Ezekiel Wenje walizuiwa kuingia katika Ukumbi wa Bunge kwa maelezo kuwa wamevaa kombati (sare zinazotumiwa na chama hicho).
Tangu Juni 17 mwaka huu wabunge wa chama hicho hawakuhudhuria mjadala wa bajeti, badala yake walikwenda kushiriki shughuli za mazishi ya watu waliokufa baada ya kutokea kwa mlipuko wa bomu wakati chama hicho kikihitimisha kampeni zake za uchaguzi mdogo wa udiwani katika Viwanja vya Soweto jijini Arusha.
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika ofisi za Kambi ya Upinzani Bungeni, Lissu ambaye alitumia dakika 36 kufafanua sababu za kutoshiriki kwa chama hicho.
“Hatukushiriki kwa sababu ya matukio yaliyotokea baada ya shambulio la bomu na kauli zilizotolewa ndani na nje ya Bunge,” alisema.
“Uamuzi huo umekuja baada ya wabunge wote wa chama hiki kukutana jana kwa saa 3, kujadili jinsi ya kushiriki katika mjadala wa kuhitimisha bajeti hiyo.”
CHANZO: www.mwananchi.co.tz

No comments:

COMMENTS

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...