SERIKALI imesisitiza kuwa itatoza Sh
1,000 kwa kila kadi ya simu inayotumika lakini pia inaangalia utaratibu
wa kufanya makato hayo kwa njia ambayo haitamuumiza mtumiaji wa simu.
Akizungumza jana jijini Dar es salaam,
Waziri wa Fedha,Dk William Mgimwa alisema kuwa kupitia tozo hizo
wanatarajia kukusanya Sh bilioni 160 kwa mwaka.
“Kupitia wawakilishi wenu na sisi
serikali kuwa sikivu, tulishauriwa na ikaonekana kwamba kuna uwezekano
wa kupata chanzo kingine cha mapato kupitia kadi za simu” alisema.
Alisema katika mapendekezo yaliyokuwa
yametolewa serikali ilishauriwa kutoza Sh 1,450 katika kila kadi ya simu
lakini baada ya kukaa na kushauriana serikali iliona ni vyema ikatoza
Sh 1,000 ili kila mwananchi aweze kumudu gharama ambapo kwa mwaka kila
mmiliki wa kadi ya simu atatozwa sh 12,000.
Alisema baadae serikali ilipokea
mapendekezo mbalimbali ili kuangalia kama hilo linaweza kutekelezeka na
walipita ngazi zote kabla halijapelekwa katika kamati za Bunge na
kushauriwa kwamba tozo hilo linaweza kufanyika kwa lengo la kukuza
uchumi hasa maeneo ya vijijini.
“Tathmini zote zimefanyika kikamilifu na
baadae suala hilo likafikishwa Bungeni ambapo pia napo lilikubalika...
inawezekana watu wanalalamika lakini ngazi zote suala hilo lilipopita
lilikubalika na ikaonekana ni sawa kutozwa sh 1,000 kwa kila kadi ya
simu” alisema.
Alisema kutokana na hilo kwa kutwa nzima
kadi ya simu itatozwa Sh 33.35 au Sh 100 kwa siku tatu ambapo serikali
inaangalia utaratibu mzuri ambao hautamuumiza mtumiaji wa simu.
Dk Mgimwa alisema fedha hizo
zitakazokusanywa zitaongeza upatikanaji wa maji vijijini, umeme pamoja
na kuboresha miundombinu katika maeneo ya vijijini.
Habari Leo
No comments:
Post a Comment